Curriculum
Course: usimamizi wa fedha
Login
Text lesson

1. Kama haujui tatizo, huwezi kupata ufumbuzi/suluhisho.

Fikiria … unacheza mechi ya mpira wa miguu. Lakini inatokea hakuna mtu anayehesabu magori yaliyofungwa. Je, itawezekanaje kufahamu ni nani mshindi?

Ama unakwenda kwa daktari na anapokuuliza ni “nini kinakusumbua”  unashindwa kusema kama ni kichwa, tumbo au mguu wako unauma. Hii itampa wakati mgumu daktari kukutibu. 
 
Kama hujui tatizo, huwezi kupata ufumbuzi wake. Hivi ndivyo ilivyo katika fedha: Ni matumaini yangu kuwa unasoma maelezo haya kwasababu unataka kujifunza namna bora ya kutumia fedha. Jambo la kwanza katika kuboresha namna bora ya kusimamia fedha…inakupasa kutambua juu ya nini unafanyia fedha zako…Kumbuka, utawezaje kukirekebisha kitu kilichoharibika ikiwa haujui mahali palipoharibika? 
Jambo la kwanza: Orodhesha matumizi yako yote ya fedha zako – yakiwemo matumizi madogo madogo (kwani huongeza gharama!). Yaani mapato na matumizi ya fedha zako zote.

Tafuta mfumo unaokufaa katika utunzaji wa mahesabu ya fedha zako. Inaweza ikawa programu fulani, ama katika simu yako ya kiganjani, katika daftari au kompyuta; hii inaweza ikafanyika siku kwa siku…Kwa chochote unachojisikia kukifanya yakupasa kukikamilisha. Hakikisha unatafuta kiwango sahihi cha maelezo juu ya kila kitu utakacho taka kukifanya: Mfano: chakula, mavazi au usafiri…ama unaweza ukachanganua zaidi juu ya chakula, kwa kutoa mchanganuo wake kati ya kununulia sokoni ama mgahawani. Hii hutegemea na namna unavyotumia fedha zako. Na kila kitu hutegemea urahisi na umuhimu wake.

Kisha, inapofikia mwisho wa juma jumlisha matumizi yote yanayofanana (mfano: chakula, n.k). kimsingi changanua kama kipato chako ni mshahara wa kila mwezi na ili kupata picha halisi juu ya matumizi yako ya mwezi unaweza kutengeneza mchanganuo huo kwa mwezi mmoja mmoja.
Hebu fikiria…unawekeza katika kampuni kubwa lakini hawawezi kukwambia wanatumia kiasi gani na kama wanatengeneza faida yoyote, je, ungeliwaamini? Hivyo, kuweka kumbukumbu juu ya kila unachotumia ndicho kitu cha kwanza na hukufanya kujiamini. Watu wengi huamini kuwa unapoanza kuweka kumbukumbu ya matumizi yako “hukufungua ufahamu”. “Sikulitambua kumbe natumia fedha nyingi juu ya kitu fulani”. Kumbuka: kama haulijui tatizo huwezi kupata ufumbuzi wake.

 

Mazoezi:

Yafuatayo ni mawazo ya namna ya kuorodhesha mapato na matumizi yako. 

  • Daftari: Unaweza ukaandika kila kinachoingia na kutoka katika daftari (hii ni kama unatumia pesa taslimu) moja baada ya nyingine na kuona ni kiasi gani unabakisha kila baada ya siku.
  • Mchanganuo: Andika kila kinachoingia na kutoka katika mchanganuo wa kimahesabu. Hii inakurahisishia kujumlisha gharama ya matumizi yako kwa wiki ama mwezi.
  • Kompyuta: Ama andika moja kwa moja katika programu maalumu ya kufanyia mahesabu katika kompyuta yako au tunza risiti za matumizi yako ama daftari lako na unakili katika programu maalumu ya kufanyia mahesabu katika kompyuta yako (tazama mfano hapa chini) au katika programu yeyote ile (hii ni kama una akaunti tofauti tofauti za benki, uwekezaji… n.k).
  • Programu: kuna programu nyingi ambazo unaweza kuzitumia kuandika kila kinachoingia na kutoka na hii inakusaidia katika kupangilia vyema bajeti yako (tutaweza kupitia hili baadaye).
  • Taarifa za Kibenki: Pakua na uziangalie.
  • Angalia na Ukague: Ni lazima mahesabu na kumbukumbu zako ziwe sawa sawa na kiasi halisi cha fedha ulichonacho mkononi. Hivyo yakupasa kuhesabu fedha zako! Kwa mfano: Unaanza siku ukiwa na dola 100 katika pochi yako,inatokea unatumia dola 40 na kubakiwa na dola 60. Hivyo inakupasa kuhesabu fedha zako na ikitokea umebakiwa na dola 58…inawezekana ulijisahau kuweka kumbukumbu ya matumizi yako.  Na kama unajikuta una dola 61, inawezekana umekosea kupiga mahesabu yako, ama kulikuwa na makosa katika kurudishiwa chenchi. Yakupasa kuandika tofauti hiyo kama “tofauti” katika daftari la kumbukumbu zako ili kuhakikisha kuwa mahesabu ya fedha zako yapo sawa na kiasi halisi cha fedha ulicho nacho mkononi. 

Kitu cha kuzingatia zaidi ni kutumia programu ambayo itarahisisha ufuatiliaji wa kila unachokifanya na kukitumia….kila siku, mwezi baada ya mwezi…ama mwaka mzima! 

 

Mwisho wa somo la kwanza. Furahia ufuatiliaji wa matumizi ya fedha zako hadi somo lijalo!